Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa Iran haina imani kabisa kwamba Israel itaheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, akisisitiza kuwa Mkataba wa Amani wa Abraham (Abraham Peace Accord) ni usaliti mkubwa dhidi ya Waislamu na Wapalestina, na kwamba Iran haitajiunga kamwe na mkataba huo.
Akizungumza katika kikao cha kidiplomasia mjini Tehran, Waziri Araghchi alibainisha kuwa historia ya Israel imejaa uvunjaji wa ahadi na ukatili dhidi ya watu wa Palestina, hivyo hakuna sababu ya kuamini kuwa itaheshimu makubaliano yoyote ya amani.
Amesema:
“Kila mara Israel inaposhindwa kijeshi au inapokabiliwa na shinikizo la kimataifa, hukubali makubaliano ya muda tu ili kupata nafasi ya kujipanga upya na kuendeleza mashambulizi mapya. Hivyo, amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa kutegemea ahadi zake.”
Araghchi pia alisisitiza kwamba Mkataba wa Amani wa Abraham, uliotiwa saini kati ya Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu, ni hatua ya kuhuzunisha na ni usaliti wa wazi dhidi ya umma wa Kiislamu, kwani unahalalisha uvamizi na ukaliaji wa ardhi za Palestina.
Akaongeza kuwa Iran itabaki imara katika msimamo wake wa kimaadili na Kiislamu wa kuunga mkono harakati za ukombozi wa Palestina na kupinga uhusiano wowote wa kawaida na utawala wa Kizayuni.
“Iran haitajiunga kamwe na makubaliano yoyote yanayopuuza haki za Wapalestina. Tunapigania amani ya kweli - amani inayojengwa juu ya haki, uhuru na heshima,” alisema Araghchi.
Your Comment